Friday, November 13, 2009

Muhimbili waanza mgomo baridi

WAFANYAKAZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana walianza kufanya mgomo baridi ili kuishinikiza Serikali kuwalipa ya nyongeza ya mishahara waliyoahidiwa tangu Julai mwaka huu.
Uamuzi wa wafanyakazi hao kufanya mgomo huo baridi unasababishwa na subira yao ya muda mrefu juu ya madai yao kugonga ukuta huku Serikali ikiendelea kuwapiga danadana.

Hata hivyo, wafanyakazi hao waliafikiana kuwa mgomo huo utaanza rasmi Novemba 28, mwaka huu kama serikali hatatekeleza makubaliano yao.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu (Tughe),tawi la Muhimbili, Nusura Barakabitse alisema mgomo uliopo katika hospitali hiyo hivi sasa ni baridi; ambapo wanafanya kazi kinyume na taratibu zao za kila siku.

Alifafanua kuwa mgomo huo ambao sasa hivi unaoendeshwa kisirisiri utakuwa wa wazi ifikapo Novemba 28, wakati wafanyakazi wanapokea mishahara.

Alifahamisha kuwa wamepanga kuanza tarehe hiyo ili waone kama serikali itakuwa imefanya marekebisho ya mishara yao au la na kwamba, wakirekebishiwa hawatagoma.

Alisema wafanyakzai wanashangaa kuona mwajiri wao ambaye ni serikali ameshinda kutekeleza madai yao ya kuongeza mishahara kwa asilimia nne kuanzia Julai, mwaka huu.
Kiongozi huyo wa chama cha wafanyakazi, alisema wafanyakazi hao wamesubiri kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote huku Serikali ikiendelea na hadithi zake kuwa madai yao yanafanyiwa kazi.
Barakabitse alieleza kuwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi kuwa wataanza mgomo, uongozi wa Tughe uliamua kuonana na uongozi wa MNH na Hazina, ambao walisema fedha za nyongeza ya mishahara zinaandaliwa.
Alisema suala la kucheleshwa nyongeza ya mshahara ya wafanyakazi wa MNH, lianza baadaya sakata lililoibuliwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), kwamba kuna wafanyakazi 364 hewa katika hospitali hiyo ambao hawatambuliki na serikali.

Hata hivyo,alisema uongozi wa Tughe unajiandaa kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili kumuelezea juu ya mgomo utakaofanyika Novemba 28, kwamba utakuwa ni mkubwa kutokana na hasira za wafanyakazi, hivyo kusababisha athari kubwa.

Source: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment